Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

WATUMISHI 43 WA NJOMBE RRH WAHITIMU MAFUNZO YA AWALI, MAHALI PA KAZI

Posted on: June 7th, 2024

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe imetoa mafunzo ya siku mbili kwa watumishi wapya wapatao 43, lengo likiwa ni kuwaelekeza kanuni, taratibu, miongozo mahali pa kazi, pamoja na utoaji wa huduma bora katika maeneo yao ya kazi, huku wakikabidhiwa vyeti kwa ushiriki wao.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa jana Juni 7 na kufungwa leo Juni 8 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, yamewanufaisha watumishi hao katika maeneo mbalimbali ikiwemo Haki na wajibu wa Mtumishi wa Umma, Kanuni za Utendaji kazi kwa Mtumishi wa Umma, Muundo wa  Uendeshaji wa Hospitali, na Uzuiaji Maambukizi mahali pa kazi.

Maeneo mengine waliyonufaika katika mafunzo nayo ni pamoja na Elimu kuhusu Usimamizi wa fedha, Manunuzi na  Ugavi, Huduma bora kwa Mteja, Mfumo unaohakikisha Usalama mahali pa kazi (5S) Mifumo ya uagizaji dawa katika Bohari ya Dawa ya Hospitali, Ujuzi kuhusu Maisha, na namna ya kukabiliana    na majanga ya moto mahali pa kazi. 

Awali akifungua mafunzo hayo hapo jana Dkt. Kwesi aligusa maeneo mbalimbali ambayo watumishi hao walipaswa kuyatilia maanani hasa katika kukamilisha maana halisi ya Mtumishii wa Umma. 

" Kuna maeneo ambayo ningependa mkayawekee mkazo, suala la mavazi na kuwa nadhifu kwa watumishi, kwani mtumishi akiwa nadhifu ni dhahiri mteja atakuwa huru kuhudumiwa naye, pia suala la vitambulisho na sare ni muhimu sana...Suala la kufika kazini kwa muda uliopangwa na serikali" Alisema Dkt. Kwesi

Alisema kuwa mbali na kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kuzifahamu taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma, pia itasaidia kuondoa migongano baina ya watumishi hao na viongozi wao katika Idara na vitengo wanavyofanyia kazi. 

 Katibu wa Afya Bi. Tekra Myumbilwa alisisitiza watumishi kutimiza wajibu wao, na kutojihusisha na matendo yanayokinzana na utumishi kwa kuwa yanaweza kuwa chanzo cha Mtumishi kuchukuliwa hatua za kinidhamu, au kufukuzwa kazi kabisa.


Naye Mratibu wa Mafunzo na Utafiti, Bw. Evaristus Makota, amewashukuru watumishi wote waliohudhuria mafunzo hayo kwa kuwa na utayari wa kujifunza kwa muda huo wa siku mbili, huku akitoa ujumbe wa kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza. 


"Tunashukuru kwa muda wote wa mafunzo mmekuwa na mwitikio na hali ya kujifunza; katika vipindi 19, ndani ya siku mbili;  hivyo nitoe wito kwenu kwa kila mmoja; ukipata muda pitia hayo yote tuliyojifunza, yatakusaidia kukukumbusha na kukufanya uendelee kuishi katika misingi na miongozo tuliyopeana katika siku hizi mbili" Amesema Makota. 

Miongoni mwa waliokuwa wawezeshaji mafunzo hayo ni pamoja na Bw. Jafary Simika, Afisa Utumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Limi Mbembela, Mkuu wa Kitengo cha Ugavi -Njombe RRH, Rehema Nyongole, Afisa Afya Kinga na Mazingira - Njombe RRH,  Evaristus Makota Mratibu wa Mafunzo na Utafiti - Njombe RRH, Benard Sapula, Mfamasia - Njombe RRH , Justine Kibona, Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu - Njombe RRH, Hassan Majaliwa, Mkuu wa Kitengo cha Afya Kinga na Mazingira pamoja na Rasuli Chihako, Afisa Fiziotherapia, na Mratibu wa Michezo - Njombe RRH. 

Mganga Mfawidhi amehitimisha mafunzo hayo leo kwa kuwataka Watumishi kuzingatia yale yote waliyowezeshwa katika mafunzo hayo, ili kuleta tija katika utoaji huduma bora za Afya.