Contact Us | FAQ | Mails | Complaints |

UJUMBE MKUBWA KATIKA HAFLA YA MAKABIDHIANO YA OFISI YA MGANGA MFAWIDHI, NJOMBE RRH

Posted on: January 26th, 2024

 Mkurugenzi Msaidizi wa Utumishi, Wizara ya Afya Bw. Daniel Temba amewapongeza watumishi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo madai ya stahiki, na miundombinu mbalimbali ikiwemo usafiri.

Temba ametoa pongezi hizo katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi leo Januari 26, kati ya aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe Dkt. Winfred Kyambile na Mganga Mfawidhi wa sasa Dkt. Gilbert Kwesi.

Licha ya pongezi hizo bado amewataka watumishi kuendelea kufuata miongozo ya Utumishi iliyowekwa na serikali kupitia wizara ya Afya, kwa kuwa serikali imewajengea miundombinu bora ya ufanyaji kazi.

“Hospitali hii ni bora kuliko Hospitali zote zilizojengwa hivi karibuni; majengo na mazingira ni mazuri na yanatia moyo kufanya kazi; mnapaswa kujivunia kwa kufanya kazi katika mazingira mazuri kama haya. Mheshimiwa Rais wetu amefanya kazi kubwa sana, tusimwangushe watumishi” amenukuliwa Bw. Temba.

Amempongeza aliyekuwa Mganga Mfawidhi pamoja na watumishi wote kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya ujenzi wa Hospitali hii, ambayo imesimamiwa tangu kujengwa kwake hadi sasa na aliyekuwa Mganga Mfawidhi, Winfred Kyambile.

“Rasmi kwa niaba ya Wizara, tunampongeza Dkt. Kyambile kwa kazi nzuri aliyoifanya; lakini kwa sababu derive naye ni abiria, tunatambua pia mchango mkubwa wa watumishi katika ujenzi wa Hospitali hii” amesema.

Miongoni mwa zilizotajwa kama changamoto miongoni mwa watumishi ni pamoja na Ukosefu wa Usafiri wa Hospitali kwa watumishi, kushuka kwa fedha za OC (other charges) ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ukosefu wa wigo wa Hospitali, hivyo kukosekana kwa usalama wa kutosha kwa watumishi na rasilimali vifaa za Hospitali, pamoja na tatizo la kukatika katika kwa umeme.

Mkurugenzi wa Utumishi Msaidizi, ameahidi kuzishughulikia changamoto hizo, ambapo ametoa mapendekezo ya kuanza na ujenzi wa wigo, kabla ya kuanza ujenzi wa majengo mengine ya huduma, kwa kuwa bado yanajitosheleza kwa sasa katika kutoa huduma.

Kuhusu suala la kukatika kwa Umeme ameahidi kuwa atalichukua na kulipeleka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili ikiwezekana, itengenezwe line maalumu kwaajili ya Hospitali, huku akitoa maagizo kwa viongozi wa Hospitali.

“Mkasimamie na kutumia mapato ipasavyo na kwa kufuata taratibu za kiserikali; lakini pia viongozi, tengenezeni mazingira ya kufikiwa na watumishi na jamii ya Njombe, ili kutatua matatizo haraka” amesisitiza.

Naye aliyekuwa Mganga Mfawidhi Dkt. Winfred Kyambile, amewaomba watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mganga Mfawidhi, Dkt. Gilbert Kwesi.

“Tangu Novemba 16, 2016 nimetumikia nafasi ya Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Njombe, tangu nikiwa katika Hospitali Teule ya Mkoa Kibena. Mpokeeni Dkt. Gilbert ana uzoefu mkubwa. Tunashukuru kwa kutupatia Daktari bingwa wa Upasuaji, kilikuwa kilio kikubwa sana kwa Mkoa wa Njombe, watumishi shirikianeni naye vizuri” amesisitiza Dkt. Kyambile.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Rufaa mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, ameishukuru Wizara ya Afya kupitia Katibu Mkuu, kwa kumwamini, hivyo akaahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na watumishi.

“Shukrani zangu ni kwa Wizara ya Afya kwa kuniamini, nimepokea kwa moyo thabiti kufanya kazi hii. Yale yote matamanio yenu tutayatimiza pamoja. Tuwe wawazi kueleza na kuweka bayana changamoto zilizopo, na yale yote tunayotamani kuyafanya basi tuyatekeleze. Sijaja kutengua Torati bali kulitimiza” amenukuliwa Dkt Kwesi.

Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa Njombe, imewakilishwa na Dkt. David Ntaindwa, ambaye ameahidi kuwa Ofisi ya Mganga Mkuu mkoa wa Njombe itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mganga Mfawidhi na watumishi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe